Tuesday, January 26, 2016
MSUKULE AKUTWA KWENYE NYUMBA YA TAJIRI MBEZI KIBAMBA.
Hali ya woga imeendelea kutanda
maeneo ya Kibamba jijini Dar na kuacha
maswali tisa kwa wananchi kuhusiana na mwanamke aliyekutwa
kwenye shimo la urefu wa futi kumi, nyumbani kwa mfanyabiashara
aliyejulikana kwa jina moja la Mtei.
HALI YA MWANAMKE HUYO
Mwanamke huyo anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 27,
aliwashangaza wakazi wa eneo hilo kwani ndani ya shimo alilokutwa
alionekana mchafu, aliyenyongea, akiwa hoi kwa njaa na mtupu kiasi
cha kudhaniwa ni msukule (mtu aliyechukuliwa ndondocha).
SIKU YA TUKIO
Ilikuwa Jumanne ya Januari 19, mwaka huu katika shimo hilo
lililojengwa na Mtei, inasemekana kuwa, shimo hilo ni kwa ajili ya
chemba ya choo lakini haijaanza kutumika kwa vile nyumba hiyo nayo
haijaanza kukaliwa rasmi na familia zaidi ya kuwepo kwa mlinzi.
Akiwa uchi shimoni.
UWAZI ENEO LA TUKIO
Kufuatia kusambaa kwa taarifa za mwanamke kukutwa shimoni
kwenye nyumba ya mfanyabiashara huyo, Uwazi kama ilivyo ada yake,
lilitinga eneo la tukio kwa lengo la kuchimba mawili, matatu kuhusu
hali halisi.
MAJIRANI WASHANGAZWA
Baadhi ya majirani wa eneo hilo walionesha kushangazwa na tukio hilo
huku wakiwa na maswali hayo tisa kuhusu mwanamke huyo ambaye
walisema si mkazi wa maeneo hayo na wala hawajawahi kumuona.
Mwanamke huyo baada ya kutolewa shimoni.
MASWALI YA MAJIRANI
Ni nani aliyemuingiza shimoni mwanamke huyo na kwa madhumuni
gani? Kwani kwa jinsi shimo lilivyo, lazima aliingizwa au aliingia kwa
kutumia ngazi.
Alikuwa akiishi kwa kula chakula gani kwani wakati anatolewa, muda
mwingi alikuwa akilalamikia njaa.
Swali la tatu ambalo majirani walikuwa nalo, mwanamke huyo aliishi
ndani ya shimo hilo kwa siku ngapi? Kwani nywele na kucha zake
ziliashiria si zaidi ya mwezi mmoja. Swali kuu, aliingia/ aliingizwa lini
na muda gani kati ya mchana na usiku?
Je, aliingizwa kwenye shimo hilo akiwa na nguo zake halafu
aliyemwingiza/ waliyomwingiza walizipeleka wapi?
Swali la tano ambalo majirani hao walikuwa wakilijadili sana ni, je!
Mwanamke huyo ni mgonjwa wa akili au ni msukule? Kama si
chochote kati ya hayo mawili, kwa nini alikuwa hapigi kelele?
Sita, majirani hao waliulizana kama siku za karibuni wamewahi kusikia
kwenye vyombo vya habari kuna mwanamke mwenye umri huo
anatafutwa? Wote walisema hawajasikia.
Wengi walisema huenda mwanamke huyo aliingizwa kwenye shimo
hilo na ‘maadui’ wa biashara wa Mtei. Lakini kama ni kweli, walikuwa
na lengo gani na walimpata wapi mwanamke huyo na akiwa katika hali
gani?
Katika mahojiano na majirani wakati bado akiwa ndani ya shimo
amekaa, mwanamke huyo aliweza kujibu maswali karibu yote, lakini
swali la anaitwa nani na ameolewa au la, yalimshinda kujibu. Ni kwa
nini?
Polisi Mbezi wanasema wamekuwa wakimpigia simu Mtei, lakini
hapokei. Ni kwa nini?
MFANYAKAZI WA MTEI SASA
Naye mfanyakazi anayeitunza nyumba hiyo, Richard Pascal
alipozungumza na Uwazi kuhusu tukio hilo alikuwa na haya:
“Ninachokumbuka mimi, Jumanne, wiki iliyopita, saa 3:00 asubuhi,
bosi wangu Mtei alikuja. Ni kawaida yake kuja na kukagua mji wake.
“Nikiwa naendelea na shughuli zangu, aliniita hapa nje. Nilipofika
aliniambia nichungulie ndani ya shimo. Nilifanya hivyo, nikashtuka
sana kumwona mwanamke akiwa mtupu huku akinikodolea macho.
“Niliogopa kwa sababu sikutarajia kama kuna mtu anaishi shimoni bila
mimi kujua wakati ndiyo nalinda hapa siku zote.”
Hali aliyokuwa nayo.
AWAITA MAJIRANI
“Niliamua kuwaita majirani. Baada ya muda mfupi watu wakawa
wamejazana hapa kila mmoja akishangaa na bosi wangu akatoa taarifa
Kituo Kidogo cha Polisi Kibamba ambapo askari walifika.
“Lakini na wao walipatwa na mshangao huku wakijiuliza ni vipi
mwanamke huyo aliingia shimoni bila kuumia wala kuvunjika?”
POLISI WAMUHOJI
“Mwanamke huyo alipohojiwa na polisi alisema ameishi humo miaka
mingi na mara nyingi alipokuwa akihojiwa alikuwa akililia chakula.
Polisi waliniomba ngazi, wakaitumbukiza shimoni kisha yeye
mwenyewe akapanda haraka mpaka nje.”
APELEKWA TUMBI
“Polisi walimchukua na kumpeleka Hospitali ya Tumbi (Kibaha mkoani
Pwani) ambako nadhani anapatiwa matibabu.”
MLINZI APATA WASIWASI
“Mpaka sasa hivi mimi napatwa na wasiwasi. Nitamuomba bosi wangu
aniongezee mtu mwingine ili tuwe wawili, kwani mimi hapa ni mgeni.
Nimekuja hapa, Desemba 9, mwaka jana.”
SIKILIZA MAHOJIANO
Uwazi lilifanikiwa kunasa mahojiani kati ya mwanamke huyo akiwa
ndani ya shimo amekaa na polisi huku wananchi wakiwa nje wakitaka
kumuokoa.
Polisi: “We, unaitwa nani?”
Mwanamke: (kimya).
Polisi: “Unakaa wapi?”
Mwanamke: “Mbezi Makabe.”
Polisi: “Umeolewa?”
Mwanamke: (kimya).
Polisi: “Umekuja lini hapo?”
Mwanamke: “Hapa kwangu.”
Polisi: Umekuja lini?”
Mwanamke: “Mi njaa inaniuma bwana.”
UWAZI NYUMBANI ANAKOISHI MTEI
Uwazi lilifika nyumbani kwa Mtei, Kibamba ya Luguruni jijini Dar, hatua
chache tu kutoka kwenye Kituo cha Mabasi Kibamba lakini
hakupatikana, Uwazi liliacha namba ya simu lakini hakupiga na
ilipopigwa, imekuwa ikiita bila kupokelewa.
UWAZI KITUO CHA POLISI
Siku hiyohiyo, Uwazi lilifika Kituo cha Polisi Mbezi ambapo askari
mmoja ambaye hakupenda kutaja jina lake kwa vile si msemaji wa
jeshi hilo, alisema mpaka sasa wanamtafuta Mtei ili kumsikia kwa kina
kuhusu tukio hilo kwa vile yeye ndiye aliyepiga simu polisi kutoa
taarifa.
“Huyo Mtei, tunamtaka hapa. Yeye ndiye aliyetoa taarifa ya mwanamke
kukutwa kwenye shimo nyumbani kwake. Lakini tulipofika
hatukumkuta. Na kila tukipiga simu yake, inaita tu bila kupokelewa,”
alisema afande huyo.
UWAZI HOSPITALINI TUMBI
Baada ya hapo, Uwazi lilifunga safari hadi Hospitali ya Rufaa ya Tumbi,
Kibaha, Pwani ambapo halikufanikiwa kumpata msemaji, lakini
muuguzi mmoja wa hospitali hiyo alikiri kupokelewa kwa mwanamke
huyo.
UWAZI LAMBANA MTEI
Juzi, Uwazi lilimpigia simu Mtei na mambo yakawa hivi;
Uwazi: “Wewe ni Mtei?”
Mtei: “Eee, unasemaje?”
Uwazi: “Tunaomba ufafanuzi kuhusu yule mwanamke aliyekutwa
kwenye shimo nyumbani kwako…”
Mtei: “Ooh! Siyo mimi, yule ni Mchaga mimi ni Muhaya, nipo Kagera.”
Uwazi likamrudia aliyetoa namba…
“Kwani si ulikuwa unaongea naye sasa hivi na akakwambia yeye si
Mtei! Nimesikia maongezi yenu, lakini alisogea mbali. Kwa hiyo sijui
zaidi.”
KAMANDA WA POLISI KINONDONI
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, ACP Christopher Fuime
alipoulizwa kuhusu tukio hilo, alikiri kulitambua na kwamba, bado
wanalifanyia uchunguzi.
Yeyote anayemjua mwanamke huyo (pichani ukurasa wa mbele) apige
simu namba 0715454656 au 0784 339616, chumba cha habari.
Source;Global Publishers
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment