Sunday, January 24, 2016

MAARIM SEIF,MH.LOWASA NA RAIS MAGUFURI MAGAZETINI LEO.

>>>>GUSA HAPA KWA HABARI NYINGINE NYINGI NA MATUKIO<<<
MWANANCHI
Wakati Eliakim Maswi aliporejeshwa kuwa katibu tawala wa mkoa

akitokea nafasi ya kaimu naibu kamishna wa Mamlaka ya Mapato
(TRA), Ikulu ilisema uamuzi huo ulitokana na kumaliza kazi maalumu,
lakini wanasiasa wamedai kuwa, amehamishwa kupunguza hasira za
Bunge.
Maswi alikuwa katibu mkuu wa Wizara ya Nishati, lakini aliondolewa
wakati wa sakata la uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta
Escrow kwa madai kuwa hakuwajibika ipasavyo kuokoa fedha za
Serikali, lakini miezi michache baadaye Ikulu ilitoa taarifa kuwa
mrasimu huyo ameonekana hakukiuka maadili katika sakata hilo
baada ya kuchunguzwa na Baraza la Maadili ya Viongozi.
Kauli hiyo ilifuatiwa na uamuzi wa Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne,
Jakaya Kikwete kumteua kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara
na baadaye Rais John Magufuli kumteua kuwa kaimu naibu kamishna
wa TRA, kabla ya kumrejesha kwenye nafasi yake mkoani Manyara
mapema wiki hii, akisema amemaliza kazi aliyotumwa.
Lakini wabunge na wasomi waliohojiwa na Mwananchi wamesema
Rais amechukua hatua hiyo baada ya kukosolewa na wanasiasa na
wadau mbalimbali wanaodai kuwa Maswi hakustahili kupewa wadhifa
huo baada ya sakata hilo la Escrow.
“Amefanya hivyo kuepuka mjadala utakaojitokeza kwenye Bunge la
Kumi na Moja kuhusu escrow,” alisema mbunge wa zamani wa
Kigoma Kusini, David Kafulila ambaye aliibua sakata hilo bungeni
mwaka 2014.
“Kuna hatari mada ya ufisadi ikaibuka kwa njia nyingine kwenye Bunge
kwa kuanza kuwazungumzia hawa wahusika ambao wamerudishwa
kwa namna ya pekee na kupewa nafasi nyeti,” alisema Kafulila,
ambaye amefungua kesi akitaka Mahakama itengue matokeo ya
ubunge na kumtangaza kuwa mshindi.
Alisema kwa nafasi aliyokuwa nayo Maswi wakati wa sakata la
Escrow, hana pa kukwepea, akidai kuwa anaweza kuhusika kwa
uzembe au kwa kukusudia.
“(Rais) Amemuondoa kupunguza Serikali kupingwa na wabunge
kutokana na kuwabeba waliohusika na kashfa mbalimbali ikiwamo
Escrow. Lakini bado kuna watu amewaacha kama (Waziri wa Nishati
na Madini, Sospeter) Muhongo na (Waziri wa Katiba) Dk Harrison
Mwakyembe, ”alisema Kafulila na kuongeza.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, ambaye alikuwa mwenyekiti
wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) iliyowasilisha ripoti ya sakata
hilo bungeni, alisema Rais hakuwa na taarifa sahihi wakati anamteua
Maswi.
Alisema hali kama hiyo ilitokea pia kwenye uteuzi wa Profesa Makame
Mbarawa ambaye kwanza alitangazwa kuwa Waziri wa Maji na
Umwagiliaji na ndani ya siku chache akahamishiwa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano.
“Hii inaonyesha hakuwa makini wakati anafanya uteuzi,” alisema
Zitto. “Hatutegemei kuona uteuzi wa kubadilikabadilika.
Awachunguze kwa makini anaowateua na nafasi anazowapa ili
kukwepa kuonekana kuwa hakuwa makini kama inavyoonekana sasa.”
Profesa Damian Gabagambi wa Chuo Kikuu cha Sokoine (Sua)
aliungana na Kafulila kwamba Rais amechukua hatua hiyo baada ya
kuona kasi anayoitaka, itaingia doa hasa baada ya watu kulalamikia
uteuzi wa Muhongo na Maswi. “Inawezekana wakati anamteua
hakuwa akifahamu vitu vingi kumhusu (Maswi), lakini baada ya uteuzi
maneno ya wadau, wasomi na watu mbalimbali yakamshtua na
kufuatilia kwa umakini,” alisema.
Profesa Gabagambi alisema uteuzi wa viongozi siyo jambo dogo hasa
unapotaka kuleta mabadiliko na mtazamo tofauti na uliokuwapo hapo
awali.
“Unaweza kuwaona viongozi wachapakazi ambao ungeweza
kuwateua, lakini kwa bahati mbaya wanatoka mkoa mmoja, hivyo
ukiwateua italeta maneno.
Hapo ndipo panapoleta tabu kidogo,” alisema Gabagambi. Profesa
Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ruaha (Ruco),
alisema lengo la Rais Magufuli ni kujenga Serikali yenye heshima,
anatamani asisikie kashfa ya aina yoyote ya ufisadi, lakini kuna baadhi
ya watu inaonekana aliwateua kabla ya kufahamu kuwa wanahusika
kwa namna moja aunyingine kwa kashfa hizo.
Alisema rais ana washauri ambao inawezekana walimpelekea taarifa
kuhusu watu aliowateua, kazipima na kuona anaweza kuleta shida
kuendelea kuwa nao hasa katika sehemu nyeti. “Siyo kwamba Rais
hasikii watu, wadau, historia ya anaofanya nao kazi inasema nini,
anasikia na hilo limeonekana katika uamuzi alioufanya kwa Maswi.
Ametafakari, amepima na kuona anatakiwa kufanya mabadiliko kama
anataka kweli mambo yaende kama anavyotaka,” alisema Profesa
Mpangala.
MWANANCHI
Siku moja baada ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Bernard Membe kusema akionana na waliokuwa
wanachama wa CCM na kuhamia upinzani anajisikia kichefuchefu,
waliokuwa makada wa chama hicho wamemshukia kwa kauli yake
hiyo.
Membe alitoa kauli hiyo hivi karibuni katika mahojiano maalumu na
gazeti hili alipotakiwa kuwazungumzia makada wa chama hicho
waliohama na kusisitiza kuwa wasipokewe endapo watataka kurudi.
Aliyekuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Goodluck Ole Medeye ambaye alitimkia Chadema, alisema kama
angesikia maneno hayo kwa mtu mwingine asingeshangaa, lakini siyo
kwa Membe.
Mbunge huyo wa zamani wa Arumeru – Magharibi, alisema Membe
anapata masilahi yake kwa kutambulika kama waziri mstaafu na
wakati anaapa kuwa katika nafasi hiyo alitumia Katiba ambayo hivi
sasa kwa kupinga yaliyomo ikiwamo uhuru wa mtu kujiunga na chama
chochote cha siasa, anakosea.
Medeye alisema kwa kauli hiyo, Membe hana haki ya kugombea nafasi
yoyote ya siasa kwa sababu haamini katika vyama vingi wakati Taifa
linaendeshwa kwa Katiba inayokubali suala hilo.
Alisema hata kauli ya Membe ya kutounga mkono uchaguzi kurudiwa
Zanzibar akitaka kufanyiwa kazi kasoro chache ni ya kinafiki kwa
sababu ameonyesha kutopenda upinzani. “Hana msimamo
hazungumzi vitu kutoka moyoni, kama kweli anakubali vyama vingi na
ana uchungu na kinachoendelea Zanzibar, kwa kuwa bado ni mjumbe
wa Nec (Halmashauri Kuu ya CCM), angemuomba mwenyekiti wake
aitishe mkutano mkuu lijadiliwe hilo na atoe anachokiamini, hakufanya
hivyo kwa sababu hakubali vyama vingi, hataki mabadiliko katika
siasa anayoitumikia, ” alisema Medeye.
Aliyekuwa kada mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombale Mwiru
alisema hawezi kujibizana na watu kwani anajua anachofanya.
Alisema anayo mawazo huru na akitaka kuzungumza jambo lolote
atafanya hivyo kwa utashi wake na siyo kujibizana na watu
waliozungumza kwa utashi wao.
Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John
Guninita alisema anamheshimu Membe kwa sababu amefanya naye
kazi katika chama hicho tawala na kumshauri siku nyingine
anapozungumza mambo kama hayo asiegemee upande mmoja.
Alisema licha ya kuwa hayo ni mawazo yake na kila mtu ana uhuru wa
kuwaza na kusema anachotaka, alipaswa apime anazungumza nini na
kwa manufaa ya nani. Guninita alisema Katiba ya nchi inamruhusu
mtu kuhama chama hata mara 10 alimradi huko anakokwenda atapata
vitu muhimu ikiwamo malengo yake binafsi, ya chama husika na
mafanikio ya Taifa.
Alisema haikuandikwa ni lazima abaki sehemu anayoamini hana
malengo nayo, au asihame kutoka chama kimoja ama kingine.
MWANANCHI
Siku moja baada ya mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC)
kuitangaza Machi 20 kuwa siku ya marudio ya Uchaguzi Mkuu wa
Zanzibar, mgombea urais, Maalim Seif Sharif Hamad na Edward
Lowassa leo wanakutana na wabunge wote kutoka vyama
vinavyounda Ukawa kutoa “tamko zito” litakalotoa mwelekeo wa hali
halisi ya kisiasa visiwani humo.
CUF, ambayo inapinga kurudiwa huko kwa uchaguzi, nayo imepanga
kufanya vikao vyake vya juu mapema wiki ijayo kuweka msimamo
wake kuhusu tangazo hilo.
Wakati hayo yakiendelea, mabomu ya machozi jana yalilipuliwa
kwenye maeneo tofauti ya Zanzibar wakati askari wa Jeshi la Polisi
wakitawanya watu waliokuwa wamekaa kwenye vikundi, kwa kuhofia
kuwa wanaweza kutumia mwanya huo kufanya vurugu.
Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha alitangaza juzi kuwa marudio
ya uchaguzi hayatatanguliwa na kampeni za wagombea wa nafasi za
urais, uwakilishi na udiwani na wala hakutakuwa na mabadiliko yoyote
ya wagombea.
Bado vyama vya upinzani havijatoa tamko kuhusu uamuzi huo wa
ZEC, lakini viongozi wa vyama vinavyounda Ukawa; Chadema, CUF,
NLD na NCCR Mageuzi wanatarajiwa kuhudhuria kikao hicho
kitakachofanyika kwenye Ukumbi wa African Dream.
Habari zilizolifikia gazeti zinaeleza kuwa awali katika kikao hicho
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ulipanga kujadili mkwamo wa
kisiasa na jinsi ya kupata suluhu, lakini baada ya ZEC kutangazaa
kurudiwa kwa uchaguzi huo, ajenda imebadilika na sasa umoja huo
utatoa msimamo wake wa mwisho kuhusu Zanzibar.
Msemaji wa Lowassa, Aboubakar Liongo na Ismail Jussa
walithibitisha viongozi hao kutua Dodoma jana jioni tayari kwa kikao
hicho ambacho kitaanza asubuhi.
Habari zaidi zinaeleza kuwa awali, Maalim Seif na Lowassa, ambaye
alikuwa Waziri Mkuu na ambaye mwaka jana aligombea urais wa
Tanzania kwa tiketi ya Chadema, watakutana na viongozi wakuu wa
Ukawa na baadaye na wabunge wote na kisha kutoa maazimio.
“Ni maazimio ambayo yanalenga kueleza ukweli kuhusu kinachotaka
kufanyika Zanzibar. Yatakuwa maazimio mazito,” alisema mpashaji
habari wetu.
Januari 20, wabunge wa Ukawa walifanya kikao cha ndani kwenye
ukumbi wa Pius Msekwa uliopo viwanja vya Bunge kuhusu hali ya
kisiasa visiwani Zanzibar na kutangaziwa kuwa wataelezwa msimamo
wa umoja huo leo.
“Watapewa mrejesho wa kikao cha mwisho kati ya Maalim Seif na
(Rais wa Zanzibar) Dk Ali Mohamed Shein. (Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman) Mbowe na mwanasheria wa Chadema (Tundu Lissu) nao
wataeleza masuala mbalimbali kuhusu Zanzibar,” alisema mtoaji
habari huyo ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.
Mwenyekiti wa NCCRMageuzi, James Mbatia alisema licha ya
kuwapo kwa mazungumzo hayo, msimamo wa Ukawa na CUF wa
kupinga uchaguzi huo kurudiwa, upo palepale.
“Kesho (leo) tunazungumza kuhusu Zanzibar. Pamoja na mambo
mengine tutatafakari hali ya kisiasa visiwani Zanzibar na nchi kwa
ujumla na baada ya hapo tutatoa maazimio yetu,” alisema Mbatia.
Alisema lengo la kikao hicho ni kuelezana kwa kina lilipo tatizo,
kupewa taarifa na takwimu sahihi. “Hatuko tayari kurudiwa kwa
uchaguzi Zanzibar, Watanzania lazima wakumbuke kuwa ukitenda
haki, amani ndipo hupatikana,” alisema. Alisema kutokana na kufutwa
kwa uchaguzi huo, Tanzania imetengwa pamoja na kunyimwa fedha
za maendeleo kutoka mataifa makubwa. “Ole wao wanaofanya
mambo haya.
Yakisababisha umwagaji damu yatawagharimu na wapo
watakaokamatwa na kufikishwa Mahakama ya Kimataifa kwa
kusababisha mauaji,” alisema Mbatia. “Suala la Zanzibar
hatukubaliani nalo kwa sababu ukishawekwa utaratibu, halafu
ukauvuruga ni fujo.
Na duniani kote dola na taasisi huundwa kwa njia ya maridhiano,”
alisema. “Mwaka 1995 na 2000 mauaji yalitokea Zanzibar lakini
mwaka 2010 hayakutokea kwa sababu ya maridhiano ya CCM na CUF.
“Leo hii Zanzibar wanarudi kulekule kwa kuwa CCM wasiposhinda
inakuwa nongwa.
Wanataka wao ndiyo washinde tu na wanadhani wao ndiyo wenye fikra
na haki tu. Kama ni hivyo kwa nini mfumo wa demokrasia uwepo?”
Wakati mkutano huo ukiandaliwa, Kaimu Mkurugenzi wa Habari na
Uhusiano wa Umma wa CUF, Jussa, ambaye amelielezea tamko la
Jecha kuwa halizingatii Katiba wala sheria. Katika taarifa kwa vyombo
vya habari, Jussa amelielezea tamko hilo kuwa “la kihuni lisilozingatia
Katiba wala sheria” na kwamba vikao vya juu vya chama hicho
vitafanyika mapema wiki ijayo kufanya uamuzi.
“Kamati ya Utendaji ya Taifa itakutana tarehe 27 Januari, 2016 na
kufuatiwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa litakalokutana Alhamisi,
tarehe 28 Januari, 2016,” inaeleza taarifa hiyo iliyotolewa na Jussa
akiongeza kuwa vikao hivyo vitafanyika kwenye ofisi za makao makuu
ya CUF zilizopo Buguruni jijini Dar es Salaam.
Taarifa hiyo inawataka wananchi ambao kinasema “waliikataa CCM
kwa kishindo Oktoba 25”, kuendelea kutunza amani na kuwa watulivu
“katika kipindi hiki kigumu na kusubiri maamuzi ya chama chao
wanachokiamini”.
Akitangaza tarehe ya kurudia uchaguzi huo juzi kupitia kituo cha
televisheni cha Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) ambako pia
Januari 28, 2015 alitangaza kuufuta, Jussa alisema kulikuwa na
ukiukwaji wa sheria na kanuni za uchaguzi.
Alisema uchaguzi huo utarudiwa ndani ya siku 90. Juhudi za kutafuta
suluhisho la kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi huo zilizomshirikisha
Dk Shein na Maalim Seif zimegonga mwamba baada ya kufanya vikao
tisa bila kuafikiana. Tayari Maalim Seif ameshajitoa kwenye
mazungumzo hayo yaliyohusisha vikao tisa
MWANANCHI
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limetoa ufafanuzi
kuhusu mavazi ya kijeshi ambayo Rais John Magufuli alivaa juzi
wakati akienda Chuo cha Maofisa wa Jeshi cha Monduli (TMA)
mkoani Arusha.
Dk Magufuli alivaa vazi hilo lenye mabaka ya rangi ya mchanganyiko
ya kijani, kahawia nyeusi na nzito, lakini haikuwa na alama za cheo
mabegani wala kifuani, jambo lililosababisha mjadala mkubwa hasa
kwenye mitandao ya kijamii.
Kilichokuwa kikihojiwa zaidi ni sababu za kutoa alama hizo wakati
akiwa kwenye taasisi ambayo utambuzi wa cheo hutegemea nishani
hizo. Msemaji wa JWTZ, Kanali Ngemela Lubinga alisema jana kuwa
hakukuwa na tatizo lolote kwa Rais Magufuli kuvalia mavazi hayo bila
alama za vyeo na wala kuyatumia wakati akihutubia wananchi.
Kanali Lubinga alisema Sheria ya Jeshi ya Mwaka 1966 (National
Defence Act) inamhalalisha Rais aliyepo madarakani kuvalia mavazi
hayo kwa kuwa ni Amiri Jeshi Mkuu.
Kuhusu magwanda hayo kutoonyesha vyeo, Lubinga alisema tofauti
na wanajeshi wengine, sare za Amiri Jeshi Mkuu hazina vyeo wala
alama yoyote mabegani.
Juzi, kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii watu walituma picha
inayomuonyesha Rais Magufuli katika mavazi hayo sambamba na
picha ya Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ambaye gwanda lake lilikuwa
na nyota nne.
Pia, picha hizo ziliwaonyesha viongozi wa zamani, Mwalimu Julius
Nyerere, Samora Machel wa Msumbiji na Kenneth Kaunda wa Zambia
wakiwa wamevalia magwanda ya kijeshi, lakini ambayo hutumiwa
kwenye shughuli za kawaida.
Picha nyingine zilimuonyesha Rais Yoweri Museveni wa Uganda,
Barack Obama (Marekani) na Paul Kagame wa Rwanda wakiwa
kwenye magwanda hayo.
Kuhusu kuvalia mavazi hayo wakati akihutubia wananchi uraiani,
Lubinga alisema alilazimika kuhutubia wakati akiwa njiani kuelekea
chuo hicho cha kijeshi cha Monduli.
“Watanzania waelewe kwamba kitendo cha Rais kuvalia mavazi ya
kijeshi si cha ajabu kwa sababu alikuwa kwenye shughuli za kijeshi na
nafasi yake ya Amiri Jeshi Mkuu inampa haki hiyo,” alisema.
Alisema Rais alikuwa anakwenda kwenye majukumu ya kijeshi, lakini
kutokana na watu kumtaka kwa kumfungia barabara, alilazimika
kusimama na kuzungumza nao kukata kiu.
“Baada ya msafara wake kusimamishwa wakati akielekea Chuo cha
Maofisa wa Jeshi, haikuwezekana kurudi ili abadilishe mavazi ndipo
arudi kuzungumza nao, ikalazimika azungumze na wananchi wake
akiwa katika mavazi hayo,” alisema Kanali Lubinga
HABARILEO
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),
Ramadhan Kailima, amesema wabunge wa Viti Maalumu
wanaruhusiwa kuwa madiwani katika maeneo wanakotoka.
Alitoa ufafanuzi huo jana, alipozungumza na gazeti hili kuhusu hatua
ya vyama vya siasa, ikiwemo CCM kuongeza idadi ya madiwani wake
kutoka kundi la wabunge wa viti maalumu, katika chaguzi za mameya
hasa jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kailima, Sheria ya Serikali za Mitaa inatambua kuwa
kila mbunge ni diwani katika eneo anakotoka, hivyo wabunge wa viti
maalumu, ni madiwani katika maeneo wanakoishi.
Kwa kuzingatia sheria hiyo, wabunge wa viti maalumu wanapoomba
nafasi hiyo ndani ya vyama na kuteuliwa, Kailima alisema, wanatakiwa
kujaza fomu namba 8D ya NEC inayoelezea maeneo wanayoishi,
ambayo ndiyo inayotumika kuwapa uhalali wa kuwa madiwani katika
maeneo hayo.
Maombi ya CCM, Chadema Kailima alisema mwishoni mwa wiki,
vyama vya CCM na Chadema waliandikia barua kwenda NEC kuomba
uthibitisho wa makazi ya wabunge wake wa viti maalumu, ili utumike
kuwaidhinisha kuwa madiwani katika halmashauri za Mkoa wa Dar es
Salaam.
Alisema CCM walikwenda na barua ikiwa na orodha ya madiwani
inaotaka wathibitishwe ukazi wao na nakala ya fomu namba 8D,
ambayo mbunge husika wa viti maalumu alijaza kabla ya kuteuliwa,
inayoonesha anuani ya eneo analoishi.
Hivyo CCM kwa mujibu wa Kailima, walithibitisha makazi na anuani ya
wabunge wanaoishi Kinondoni, wakajiridhisha kisha wakachukua
fomu yenye majina ya wabunge wote wa viti maalumu na kuweka
alama ya tiki katika majina ya wabunge wanaostahili kuwa madiwani
katika Halmashauri ya Kinondoni.
Alisema baadae Chadema walikwenda NEC na barua, lakini bila nakala
ya fomu namba 8D, hata hivyo kwa kutumia fomu hizo zilizopo NEC,
wakathibitisha wabunge wa viti maalumu wa chama hicho waliokuwa
wakazi na wasio wakazi wa Kinondoni, mbele ya Mwenyekiti wao
Freeman Mbowe na ofisa wao mmoja.
Kailima alisema kabla ya Mbowe kuondoka, aliomba kuthibitisha pia
wabunge wa viti maalumu ambao ni wakazi wa Ilala bila kuwa na
barua, ambapo aliruhusiwa kuthibitisha.
Alisisitiza kuwa kazi hiyo ya kuthibitisha ukaazi wa wabunge wa viti
maalumu, ili kutambua wanakoweza kuwa madiwani, inafanywa na
NEC kwa kuwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi), hawana uwezo kutoa uthibitisho huo.
Hivi karibuni, wakati wa uchaguzi wa Meya wa Kinondoni, vyama vya
upinzani vililalamika kuburuzwa katika uchaguzi huo, kwa madai kuwa
CCM ilitaka kuongeza madiwani wa Viti Maalumu tisa, kutoka kundi la
wabunge wa viti maalumu.
Vyama hivyo vilidai kuwa, hatua ya wabunge hao wa viti maalumu
kuwa madiwani wa viti maalumu Kinondoni, ni uchakachuaji wa wazi
wa kura za kumpata Meya wa manispaa hiyo.
HABARILEO
Bidhaa mbalimbali zilizoingizwa nchini kutoka Marekani kwa ajili ya
kutolewa msaada kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime
zimeteketezwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), kwa sababu ya
kutofaa kwa matumizi ya binadamu.
Shirika hilo pia limeteketeza nepi zinazotumika mara moja na
kutupwa, ziitwazo Smart Baby, kwa kuwa hazikidhi viwango vya ubora
vinavyotakiwa na kwa sababu zimekwisha muda wa matumizi.
Akizungumza baada ya bidhaa hizo kuteketezwa katika dampo la
Pugu Kinyamwezi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam juzi, msemaji
wa TBS, Roida Andusamile alisema bidhaa zote zina thamani ya Sh
milioni 20.
Kwa mujibu wa Andusamile, wakati bidhaa zilizoingizwa kwa ajili ya
Halmashauri ya Tarime zililetwa zitolewe msaada kwa wahitaji kwenye
eneo hilo, na nepi ziliingizwa nchini ili ziuzwe.
Aliitaja kampuni iliyoingiza nepi hizo kutoka China kuwa ni Chaoming
& Xlambin Chen, iliyolenga kuzisambaza katika soko la ndani na kwa
faida.
Andusamile alisema, “kwa kawaida bidhaa mbalimbali zinapoingizwa
nchini kutoka nje kwa ajili ya biashara, kupitia katika mipaka yetu,
bandari na viwanja vyetu vya ndege hukaguliwa na maofisa wa udhibiti
ubora kutoka TBS, ili kujiridhisha endapo zinafaa kwa matumizi au la”.
Alisema baada ya kukagua mizigo hiyo katika bandari ya Dar es
Salaam na kupima sampuli kwenye maabara husika za shirika hilo,
yalibainika mapungufu kadhaa, ikiwemo kwisha kwa muda wa
matumizi.
Ofisa Udhibiti Ubora wa TBS, Salome Emmanuel alieleza kuwa, mbali
ya muda wa matumizi ya nepi hizo kwisha, vipimo vya sampuli za
bidhaa hiyo vilionesha kuwa hazifai kutumiwa kuvalishwa watoto, kwa
sababu zina madhara kwa afya zao.
Bidhaa za msaada ambazo watu wa Marekani wanaelezwa kuchanga
ili kusaidia wahitaji Tarime, ambazo hata hivyo ziliteketezwa ni losheni
za watoto, sabuni za maji kwa ajili ya kunawa mikono, dawa za meno
aina ya Colgate na Crest.
Nyingine ni dawa za kusukutua mdomo ili usinuke, sabuni za kuoshea
nywele pamoja na sabuni za maji za kuogea. Ilielezwa kuwa bidhaa
hizo zilibainika mwishoni mwa mwaka jana, na kwamba zilizoingizwa
kibiashara ziliteketezwa kwa gharama za kampuni iliyoagiza huku za
msaada zikiteketezwa na TBS.
HABARILEO
Serikali imeombwa kuwaruhusu wafanyabiashara wa nafaka
waliopewa vibali vya kufuata mahindi katika Maghala ya Hifadhi za
Chakula ya Taifa (NRFA) kuwauzia mahindi na siyo unga wa sembe tu
katika wakati wa kipindi hiki cha kukabiliana na upungufu wa chakula
katika maeneo yao.
Ombi hilo lilitolewa juzi na baadhi ya wananchi katika kijiji cha Zanzui
wilayani humo wakati wakizungumza na waandishi wa habari
waliotembelea kijiji hicho kujionea jinsi wanavyokabiliwa na upungufu
wa chakula.
Walisema kuwa kitendo cha serikali kuwaagiza wafanyabiashara hao
kuyasaga mahindi hayo na kuwauzia unga kwa bei elekezi ya shilingi
900 kwa kilo badala ya mahindi, kunawafanya waendelee kukabiliwa
na upungufu wa chakula kwani wengi wao wanapenda kununua
mahindi badala ya unga.
“Serikali yetu imefanya vizuri kuwapatia vibali na kuwaruhusu hawa
wafanyabiashara kununua mahindi hayo kwa bei nafuu huko
Sumbawanga hadi kuyaleta hapa wilayani kwetu Maswa, lakini pia
tunaomba iwaruhusu ili waweze kutuuzia mahindi kwa bei
itakayopangwa na serikali na siyo unga,”alisema Yunge Lutonja.
Walisema kuwa wakinunua mahindi yatawawezesha kumudu njaa
inayowakabili, ikiwa ni pamoja na hata kupika makande badala ya uji
na unga tu huku wengine wakilalamikia kuwa katika maeneo yao ya
vijijini huwa hawatumii unga wa sembe isipokuwa unga wa dona.
Mfanyabiashara wa nafaka Thomas Ndaki ambaye pia ni mmiliki wa
Kiwanda cha Kusaga na kukoboa nafaka cha Ndaki Posho Mill
kilichoko katika kijiji cha Zanzui wilayani humo alisema kuwa licha ya
changamoto za kusafirisha mahindi hayo kutoka katika maghala ya
Taifa yaliyoko katika mikoa ya Katavi na Rukwa lakini wanakabiliwa na
malalamiko ya wananchi kutaka wauziwe mahindi badala ya unga.
NIPASHE
Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT), kimesema gharama ya
kumsomesha mwanafunzi wa urubani na wahandisi wa ndege ni
Sh.milioni 10 hivyo kimeiomba serikali kupitia Bodi ya Mikopo iweze
kuwasaidia wanafunzi wanaochukua kozi hizo.
Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Chuo cha
Usafirishaji Mhandisi Dk. Zacharia Mganilwa, wakati wa uzinduzi wa
‘Banda’ la ndege litakalotumika katika mafunzo ya wahandisi wa
ndege na marubani.
Alisema gharama hizo ni kubwa kulinganisha na kozi nyingine
zinazotolewa hapa nchini.
Alisema Bodi ya Mikopo imekuwa ikitoa mkopo usiozidi Sh. milioni 1.5
kwa mwanafunzi ambaye ada yake ni Sh. milioni kumi.
Mganilwa alisema gharama kubwa zimekuwa zikibebwa na mzazi,
zaidi ya Sh. milioni tisa.
“Sh. milioni tisa ambazo anatakiwa alipe mzazi imekuwa kwa kiasi
fulani changamoto kwao hivyo ninaomba bodi ya mikopo iweze
kuliangalia suala hili, waongezewa hata kidogo,” alisema.
Mganilwa aliongezea kuwa kwa hivi sasa marubani wengi na
wahandisi wa ndege wamezeeka na wengine kustaafu hivyo kuiacha
sekta ya anga kuwa na Watanzania wachache na wengi wageni.
“Mipango na mikakati yetu mikubwa ni kuona tunazalisha watanzania
wengi kabisa katika eneo hili la mafundi wa ndege na marubani,
hatutaki kuachia wageni tu waweze kuajiliwa katika sekta hii ya anga
nchini,” alisema.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Faustine Kamuzola, alisema
serikali itatoa kila aina ya msaada kwa NIT ili kiweze kuzalisha
marubani na wahandisi wa ndege wa kutosha katika kukuza sekta ya
anga nchini.
Profesa Kamuzola alisema serikali itashirikiana na Sekta binafsi katika
kukisaidia chuo hicho kiweze kufikia malengo yake ya uzalishaji wa
rasilimali watu katika sekta ya usafirishaji.
“Tumesikia kutoka kwa mkuu wa chuo hiki kuwa ada ya kumfundisha
rubani wa ndege ama mhandisi ni Sh. milioni kumi, lakini tukimpeleka
mwanafunzi nje ya nchi tutapaswa kulipa ada ya zaidi ya Sh. milioni
100, sasa serikali imewasikia,” alisema.
Aliongeza kuwa kwa kutoa mafunzo haya kwa gharama ya bei nafuu
kabisa, ana imani kwamba Watanzania wengi wenye nia ya kusomea
urubani na uhandisi wa ndege watajiunga na chuo hicho.
NIPASHE
Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imeshauriwa kuondoa kasoro
zilizojitokeza katika uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana kabla ya
kufanyika kwa uchaguzi wa marudio Machi 20 mwaka huu.
Ushauri huo umetolewa kwa nyakati tofauti na baadhi ya wagombea
wa Urais wa Zanzibar, wanasheria na  wananchi walipokuwa
wakizungumza na Nipashe Mjini Zanzibar baada ya tume kutangaza
rasimi kufanyika kwa uchaguzi huo Machi 20 juzi.
Mgombea wa urais wa Chama cha AFP, Soud Said Soud alisema
kuwa ili uchaguzi uwe huru na wa haki lazima kasoro za kiutendaji
zilizojitokeza na kusababisha matokeo ya uchaguzi kufutwa zifanyiwe
kazi ili kuepusha kujirudia kwa kasoro ikiwemo kuongezeka kura
katika masanduku kinyume na idadi ya watu waliosajiliwa kwenye
daftari la wapiga kura katika vituo vya uchaguzi.
Alisema hatua hiyo ndiyo njia pekee itakayosadia kufanyika kwa
uchaguzi huru na wa haki na kumaliza tatizo la uchaguzi Mkuu wa
Zanzibar.
Soud alisema ni lazima kwanza wananchi wote wenye sifa wapate
nafasi ya kuhakikisha wanashiriki kupiga kura bila ya kuwepo vikwazo
na mazingira ya vitisho.
“Tume ya uchaguzi lazima wasimamie na kuondoa kasoro
zilizojitokeza katika kuchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana, kabla ya
kufanyika uchaguzi wa marudio Zanzibar,” alisema Soud.
“Vitendo vya udaganyifu na mizengwe havikubaliki katika utaratibu wa
kupata viongozi waliochaguliwa kidemokrasia na wananchi.”
Mgombea urais wa Zanzibar kupitia chama cha ADC, Hamad Rashid
Mohamed, alisema uchaguzi uliofutwa ulitawaliwa na vitendo vya
udaganyifu katika vituo vya wapiga kura jambo ambalo linahitaji
kuangaliwa na ZEC kabla ya kufanyika uchaguzi mpya.
Hata hivyo, alisema kuwa mfumo mzima wa muundo wa Tume ya
Uchaguzi Zanzibar kikatiba unahitaji kuangaliwa upya kwa kufanyiwa
marekebisho ya kikatiba baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu.
Alieleza kuwa marekebisho ya Katiba yaliyofanyika na kuingiza
wajumbe wa tume wanaotokana na vyama vya siasa, kumeongeza
matatizo mkubwa na kukwamisha utekelezaji wa majukumu ya tume
hiyo.
Alisema tatizo la wajumbe wa ZEC kutawaliwa na utashi wa vyama
katika utekelezaji wa majukumu yao kumechagia kwa kiasi kikubwa
kujitokeza kwa matatizo na kulazimika uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka
jana kurudiwa Visiwani humo.
Aidha alisema sheria ya kuzuia maamuzi ya Tume ya Uchaguzi
kuhojiwa Mahakamani imepitwa na wakati kwa sababu inawanyima
wapiga kura uhuru wa Kikatiba wa kutumia mahakama, sheria
zinapovunjwa na tume hiyo.
Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS) Omar Said Shaban
alisema kurudiwa kwa uchaguzi Zanzibar sio ufumbuzi wa kumaliza
mgogoro wa mkwamo wa uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.
Alisema njia pekee ya kumaliza mgogoro wa uchaguzi ni kurudi katika
hoja ya msingi ya kufutwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu; kuangalia
kama uchaguzi huo ulikidhi matakwa ya kisheria na Katiba kabla ya
kufutwa matokeo na Mwenyekiti Jecha Salim Jecha Oktoba 28
mwaka jana.
Waangalizi wa kimataifa kutoka ndani ya Afrika na Ulaya walitangaza
kuwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 ulikuwa huru na wa haki kabla ya
kufutwa siku chache baadaye na mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salum
Jecha.
“Kabla ya Mwenyekiti kutangaza tarehe ya uchaguzi alitakiwa kusema
kifungu gani cha Katiba na sheria kimempa uwezo wa kufuta matokeo
na kuitisha uchaguzi wa marudio,”alisema Shaban ambaye pia Wakili
wa Mahakama kuu ya Zanzibar.
NIPASHE
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),
Frederick Shoo, amesema kasi ya Rais John Magufuli, ya kutumbua
majipu inaridhisha na amemtaka akaze kamba kwani watanzania wako
nyuma yake.
Aidha, Askofu Shoo amewasihi viongozi wenzake wa dini na
madhehebu tofauti kuungana kumuombea Rais Magufuli ili
kumnusuru na jambo baya kwasababu kazi anayofanya ni ngumu na
inahitaji maombi.
Aliyasema hayo jana wakati akifanya mahojiano maalumu na gazeti
hili kuhusu siku 80 za Rais Magufuli Ikulu.
Kwa tathmini ya Askofu Shoo, Magufuli ameonyesha uongozi mzuri
na ushupavu, na ni kiongozi anayepaswa kuigwa na marais wengine
duniani.
Alisema anafurahishwa na kasi ya utendaji kazi ya Rais kwasababu
ndani ya muda mfupi ameonyesha umahiri kwa kuokoa mabilioni ya
fedha zilizokuwa zikitafunwa na “wezi”.
Askofu Shoo alisema kazi ya Rais Magufuli inatia moyo kwa taifa na
kanisa kwa ujumla, hivyo alimuasa aendelee na kasi hiyo kuibua
ufisadi ambao ulikuwa ukisababisha kupotea kwa mabilioni.
Alisema wakati wa uongozi wa Hayati Mwalimu Julias Nyerere,
uchumi ulikuwa imara na nchi ilikuwa ikijiendesha kwa rasilimali
zilizoko, lakini baada ya kupita utawala wake mambo yamekuwa
tofauti.
Alisema haijawahi kutokea katika historia ya nchi kwa kiongozi
mkakamavu kama Magufuli kujitoa kwa maslahi ya taifa kwa kufichua
wezi na kuwafukuza kazi kwani kwenye serikali zilizopita
hawakuguswa.
“Labda niseme tu inawezekana Mungu amemwonyesha njia mtumishi
wake Magufuli, kwa makusudi ili afichue mambo ambayo
yakiboreshwa na kusimamiwa yataweza kuibadilisha nchi na kuwa
miongoni mwa nchi za kuigwa kupitia ukuaji wa uchumi,” alisema
Askofu Shoo.
Alisema anatarajia kutoa tamko lake mwanzoni mwa wiki ijayo kuhusu
utendaji kazi wa Magufuli katika hatua za mwanzo za utawala wake,
na kuwasihi viongozi wa dini mbalimbali kuungana katika maombi ili
kumnusuru na jambo baya dhidi yake.
Alipoingia tu madarakani, Magufuli alisababisha mtikisiko mkubwa
ndani ya Mamlaka ya Bandari (TPA) na kwenye Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) baada ya kubaini mianya ya ukwepaji wa kodi hivyo
kulazimika kuchukua hatua kali ikiwemo kuwasimamisha kazi vigogo
kadhaa wa mamlaka hizo mbili.
Miongoni mwa vigogo ambao walianza kuonja chungu ya serikali ya
Rais wa tano ni pamoja na Kamishna Mkuu wa Mamalaka ya Mapato
Nchini (TRA), Rashed Badi aliyesimamishwa kazi pamoja na vigogo
wengine saba walikamatwa na polisi akiwemo Kaimu Kamishna wa
Forodha na Ushuru wa Bidhaa, Tiagi Masamaki, kutokana na kutolewa
kwa makontena 329 yaliyotoka bila ushuru.
Katika sakata hilo zaidi ya wafanyakazi 40 wa TRA walishikiliwa na
Jeshi la Polisi kuhusina na tuhuma hizo ambazo zimeisababishia
serikali hasara ya mabilioni ambapo pia Magufuli alivunja Bodi ya
Mamlaka ya Bandari.
Mbali na kuvunja bodi hiyo, pia alitengua uteuzi wa Mwenyekiti wa
Bodi hiyo, Mhandisi Profesa Joseph Msambichaka na kumsimamisha
kazi Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Shaaban Mwinjaka kwa
kushindwa kusimamia utendaji wa TRL na TPA.
Wengine waliokwisha kumbana na rungu la Rais Magufuli ni aliyekuwa
Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
Takukuru, Dk. Edward Hoseah, ambaye ilielezwa kuwa Rais
hakuridhishwa namna taasisi yake ikitekeleza majukumu na
kushindwa kukabiliana na vitendo vya rushwa hususani kwenye
upotevu wa mapato ya serikali katika bandari ya Dar es Salaam.
NIPASHE
Mbunge wa Jimbo la Mlalo wilayani Lushoto Mkoani Tanga (CCM)
Rashid Shangazi amesema ataishauri serikali kufungua mpaka wa
Tanzania na Kenya uliyopo  Kivingo Kata ya Lunguza Wilayani Lushoto
kwa lengo la kuwawezesha wakulima Jimbo hilo kuuza mazao yao
nchi hiyo ya jirani.
Shangazi alisema kuwa suala la kero ya soko kwa wakulima wa Kata
ya Lunguza ni kubwa na kwamba mazao ya kilimo ikiwemo
mbogamboga yamekuwa tatizo kwa wakulima kuuza nchini Kenya
ambapo kuna soko la uhakika.
Alisema kwa serikali kufungua mipaka hiyo ndio itakuwa njia pekee ya
kuweza kuwapa soko la uhakika wakulima wa kilimo cha
mbogamboga na mazao mengine Jimboni humo ili waweze kunufaika
nacho kuliko ilivyokuwa sasa.
Hata hivyo Shangazi alibainisha kuwa sambamba na hilo kazi nyingine
atakayoshughulikia ni ukarabati wa barabara ya kutoka Kata ya Mtae
hadi Mnazi ambayo itaanza kwa njia ya changarawe ili kuhakikisha
miundombinu inaimarika na  kuweza kupitika nyakati zote.
“Naahidi  kuhamasisha utalii kwenye Jimbo hilo kwa kutafuta
wawekezaji watakaoweza kujenga mahotel  kutokana na Jimbo hilo
kupakana na misitu ya asili na Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi ambayo
itasaidia kutoa ajira kwa wananchi na kukuza pato lao na jamii kwa
ujumla “alisema Shangazi.
Aidha pamoja na hayo aliwataka wananchi wa jimbo hilo kuhakikisha
wanashirikiana bega kwa bega ili kusukuma kasi ya maendeleo yao
kwa kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali ambazo zinawakabili.
Akizungumzia namna atakavyoweza kukabiliana na changamoto
zilizopo kwenye sekta ya Afya, Shangazi alisema atahakikisha
anaongeza majengo ya vituo vya afya ili kuweza kuzipatia ufumbuzi
changamoto zilizopo za uchache wake.
Hata hivyo alisema mipango yake kwa vijana ni kuhakikisha kila kijiji
kinapewa shilingi milioni 50 kupitia waratibu kata ili kuunda vikundi
vya wajasiriamali 10-30 ili  waweze kujiendeleza sambamba na
kujikwamua kupitia uchumi wao.

No comments: